Lindi la maangamizi
Tunaogelea katika bahari iliyojaa vitisho kochokocho vya maangamizi. Kila uchao, ni visa na mikasa kuhusiana na jinsi bahari hii inavyozidi kuchafuka. Machafuko ya kila aina. Ugaidi, ajali za barabarani, ubakaji, wizi wa mabavu, ushoga na usagaji ni mifano tu ya machafuko hayo. Waogeleaji wanaelekea kuzama na wanaonekana wakitapatapa kwa dhiki isiyokuwa na kifani. Nao wanyama walio katika bahari hii wamejitoa mhanga kutumeza wazimawazima tusionekane tena. Watuzike na tusahaulike matumboni mwao katika jitihada za kusitisha njaa walizo nazo.
Mnyama anayeongoza katika orodha hii ni yule aitwaye “dawa za kulevya”. Kaskazini wakimzika Jonna aliyeuawa na pombe haramu, kusini wanamtibu Kalulu aliyepagawa kwa kuvuta bangi huku mashariki wakisumbuliwa na watoto waliotelekezwa na wazazi waliozama ulevini. Sijakutajia magharibi ambako kizazi kinaelekea kuangamia kwani wanaume wa huko ni majongoo wasioweza kuukwea mtungi. Majembe yao yamekuwa kama mashoka yasiyokuwa na mipini na hivyo basi hayawezi yakakata. Makaburi yameshiba kwa wafu kutokana na maafa yanayosababishwa na dawa hizi hususan pombe haramu. Ni nani atakayetunusuru kutokana na lindi hili la masaibu? Ni ajabu kubwa kuona kwamba, hata wasomi wenye akili zao tambuzi wameachwa vinywa wazi baada ya kupata makali ya anasa hino. Kweli “ anasa hunasa.” Kumbukeni kwamba binadamu huitwa razini kwa uwezo wake wa kuchamganua na kupambanua mambo.
Magari barabarani yamegeuka na kuwa masanduku ya mauti. Ukiabiri gari la uchukuzi wa umma au la binafsi, lako linasalia kuwa dua kwa Jalali kwani hujui kama gari hilo litatafuna masafa na kukufukikisha uendako salama salimini. Ni kana kwamba ziraili amekita kambi katika barabara zetu. Kila kukicha, kunaarifiwa mauko yanayotokana na ajali za barabarani. Madereva wamekosa kumakinika huku kila mmoja akionekana kutojali wengine wanaotumia barabara hizo. Magari yanaendeshwa kwa kasi ya umeme. Magari ya uchukuzi yanayopakia abiria kama magunia ya viazi vibovu. Magari makuukuu yasiyokuwa na hali. Magari yasiyosikia amri ya usukani wala breki. Nao wale wanaostahili kuhakikisha urazini barabarani, wamepagazwa na kadhongo ya hamsini na mia. Nasi, sisi wenye kubebwa, tumekuwa kama kondoo wanaoelekezwa machinjioni pasi kuuliza swali. Ongokeni muwe watu wenye utu wala si vitu vyenye kutu.
Siku zote, machozi hayatukauki machoni kutokana na adhari za ugaidi. Tunaishi roho mikononi tusijue ni lini nduli hawa watatuvamia. Wasiposafirisha watu kuzimuni kwa vilipuzi, basi watatumia mitutu ya bunduki. Kiini hasa cha mauaji haya kimesalia kuwa kitendawili kikuu kwa waliohai na hata wafu. Swali langu ni je, ni nini hiki cha mno ambacho mja hunufaika nacho kwa kumsababishia mwenzake mauti? Mali na mamlaka yanayopatikana na kunadhifishwa kwa damu ya wengine humfaa mhusika kwa kiasi gani? Nawatuma mkawaarifu waovu hawa kwamba siku yao ya adhabu ipo, na kama haipo duniani, kunayo ahera. Na kwa sababu wenye lugha husema kwamba ‘jifya moja haliinjiki chungu’, tunafaa basi kushirikiana bega kwa bega ili kukabiliana na mahasidi hawa.
Ninagura ulingoni mimi kwenda kutafuta hifadhi. Niliyoyasema yatafakarini na myapige msasa iwapo mnatazamia kwenda mbali. Ukweli mchungu ni kwamba, tukijitia hamnazo bila shaka tutazama katika lindi hili la maangamizi. Angazeni macho nayo masikio myatoe nta, ili muweze kuona na kusikia. Nafsi yangu haitakuwa nafuu iwapo mtayabeza haya na kuyatupilia mbali kwani majuto yatawaandama duniani na ahera.
Author:Wambugu Yusuf
MKU Thika